Ali Kiba, Diamond Platnumz Kimenuka Hatari...

Kimenuka! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mafahari wawili wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kudaiwa kutupiana vijembe vya kufa mtu baada ya kuwepo kwa madai ya Kiba kuhujumiwa.

Kwa mujibu wa chanzo makini, ili kuweka hujuma ya kibiashara, hivi karibuni, pamoja na kukanusha mara kadhaa kutokuwa na tatizo na Kiba, Diamond alidaiwa ‘kutengeneza’ kwa makusudi penzi la mwigizaji Jacqueline Wolper Massawe na msanii wa Wasafi Classic Baby (WCB), Rajabu Abdulhan ‘Harmonize’ kisha kuvujisha video ya uhusiano huo mpya siku ambayo Kiba alikuwa akiuachia wimbo wake mpya wa Aje (Jumamosi iliyopita), lengo likiwa kuhamisha upepo mashabiki kutoka kwenye wimbo mpya na kujali mapenzi ya wawili hao.

“Ni hujuma ya kibiashara, Diamond na uongozi wake wameamua kumfanyia Kiba ili wimbo wake ukose kiki kwa watu,” kilidai chanzo chetu.


VIJEMBE VYATAWALA
Hata hivyo, kwa mujibu wa mmoja wa mameneja wa Kiba ambaye hakupenda jina lichorwe gazetini, amemtupia vijembe Diamond kwa kudai licha ya hujuma hizo lakini hawawezi kumgusa Kiba.
“Wanajisumbua, kizuri huwa kinajiuza chenyewe na huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono. Wameingiza kiki zao lakini msimu huu hazifui dafu. Wimbo (Aje) umepokelewa vizuri na una mafanikio makubwa hadi sasa.


AZUNGUMZIA MKATABA
“Kuonesha kwamba Kiba amekubalika, ndani ya muda mfupi baada ya wimbo huo kuruka hewani, amelamba mkataba na kampuni ya kimataifa ya Sonny Music. Sasa hapo ndipo utakapoona Ngoma ya Kiba imekubalika kiasi gani, hawamuwezi huyu,” alisema meneja huyo.

KEJELI SASA!
Kama hiyo haitoshi, meneja huyo alizidi kutupa vijembe kwa Diamond kwa kueleza kuwa Kiba ni mkongwe hivyo kamwe hawezi kulingana naye kimuziki.

“Diamond hamuwezi Kiba, ameanza kuimba wakati Diamond bado hajawa msanii. Ameshafanya mengi kwenye huu muziki kuliko huyo Diamond, unakumbuka dili la One 8, Kiba aliungana na mastaa wakubwa katika project iliyokuwa chini ya msanii mkali duniani, R-Kelly (Robert Sylvester Kelly), Watanzania wanajua,” alisema meneja huyo.

KIBA HUYU HAPA
Alipoulizwa Kiba kuhusiana na vijembe na kejeli hizo anazodaiwa kuzitupa kwa mpinzani wake (Diamond), alisema ishu hiyo isiitwe vijembe badala yake ieleweke kwamba ndiyo ukweli.
“Siyo vijembe wala majungu. Huo uliosikia ndiyo ukweli wenyewe,” alisema Kiba.
TEAM DIAMOND WAJIBU MAPIGO
Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, wafuasi wa Diamond waliojipa jina la Team Diamond walicharuka kusikia msanii wao amehusishwa na hujuma za ‘kumuua’ Kiba kibiashara.
“Hana lolote huyo, Diamond ameshafanya makubwa sana ndani ya muda mfupi kumzidi yeye ndiyo maana anatapatapa kwa sababu nani asiyejua kuwa Diamond yupo fasta katika kuona fursa kuliko Kiba?
“Wolper na Harmonize wapo penzini kwa matakwa yao na si kwa kumuua Kiba, hana jipya,” aliandika mmoja wa wafuasi wa Diamond kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram.


DIAMOND ANASEMAJE?
Jitihada za kumpata Diamond ili azungumzie suala hilo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kutopatikana hewani hadi tunakwenda mitamboni lakini meneja wake, Babu Tale alipoulizwa kuhusu suala hilo, alicharuka:

Risasi Jumamosi: Tale tuambie, hivi kuna ukweli wowote kwamba Diamond na timu yako mlipanga kumzima Kiba alipokuwa anatambulisha ngoma yake mpya kwa kutupia video inayoonesha uhusiano wa Wolper na Harmonize?

Tale: “Siyo kweli. Hilo swali ni la kipuuzi. Sikiliza, ngoja nikuunganishe na bosi wako ili asikie unavyoniuliza. Nakata halafu nakupigia.
Hata hivyo, Babu Tale hakufanya hivyo na alipopigiwa tena, simu yake haikupatikana.

WOLPER AFUNGUKA
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta Wolper ili kujua kama ni kweli ametumika kumfifisha Kiba kimuziki ambapo alisema si kweli kwani penzi lake na Harmonize limetoka katika mioyo yao.
“Hakuna kitu kama hicho. Sisi tumependana wenyewe wala hatujashinikizwa na mtu yeyote kuvujisha penzi letu eti ili kumfanya fulani afifie! Kama imetokea limevuja wakati ambao huyo Kiba naye ametoa wimbo itakuwa tu imetokea lakini si kwamba tumedhamiria,” alisema Wolper huku simu ya Harmonize ikiita bila kupokelewa.

Ugomvi wa Diamond na Kiba ni wa muda mrefu ambapo huwa na msimu kwani kuna wakati unachachamaa kama sasa na kipindi kingine unapoa na hakuna anayejua hatima yao.

Comments

Popular posts from this blog

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 2 Exam Answers 100% 2016

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 3 Exam Answers 100% 2016

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 1 Exam Answers 100% 2016