Mkenya Afunga Ndoa na Mwanaume Mwenzake
Bw. Ben Gitau (33) na Bw. Steve Damelin walioana wiki iliyopita huko Ann Arbor, Michigan, Marekani, Jumamosi alasiri ambapo baada ya tukio hilo wawili hao walionekana wakibusiana na kukumbatiana ambapo marafiki na wanafamilia walipiga vigelegele na kushangilia.
Hata hivyo, mshauri mmoja wa masuala ya kifamilia , Mchungaji Philip Kitoto wa International Christian Centre, Nairobi,alilaani ndoa hiyo akisema: “Kiutamaduni na kwa mujibu wa Bibilia, ndoa na kujamiiana kati ya watu wa jinsia moja ni dhambi.”
“Biblia iko wazi kwamba Mungu alituumba kwa taswira yake; mme na mke. Katika kitabu cha Mambo ya Walawi 18:22 Mungu anamwonya mwanaume kutofanya ngono na mwanaume mwenzake kama anavyofanya na mwanamke.”
Bw. Kararu Ririe, rafiki wa karibu wa wanandoa huyo ambaye ni Mkenya aliyewahi kukiri kwamba ni shoga anayeishi California, Marekani, alitume ujumbe kwenye mtandao wa twitter baada ya ndoa hiyo akiandika kwamba: “Jioni hii nilimpongeza rafiki yangu, Ben na mumewe Steve, kwa ndoa yao. Ni jambo adimu kwa Mkenya kuwa jasiri kiasi hicho. Hongera.”
Gitau alikuwa anaishi Atlanta, Georgia, kabla ya kuhamia California. Kwa mujibu wa mwanafamilia mmoja aliyezungumza na gazeti la Daily Nation, Gitau alikutana na mchumba wake huko Atlanta ambako Damelin alikuwa mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo cha Teknolojia cha Georgia.
Katika kulaani tukio hilo, Mchungaji Kitoto alisisitiza kwamba tendo la ndoa kati ya mwanamme na mwanamke liliwekwa kwa ajili ya uzazi.
Ndoa za jinsia moja zilihalalishwa katika Jimbo la Michigan mwaka jana mwezi Julai na Mahakama Kuu ya Marekani iliyoondoa sheria zinazopinga ndoa za watu wa jinsia moja mradi tu wawe wanapendana.
Comments
Post a Comment