Skip to main content
NAMNA PEKEE YA KUEPUKA MAUMIVU KATIKA MAPENZI
Siku zote mapenzi yanapofika ukomo huwa na visa kibao hali inayopelekea maumivu yasiyokwepeka, hivyo basi kwa kuliona hilo Mtembezi Mahaba leo imekuandalia njia pekee za kukuepushia maumivu yasiyokuwa ya lazima katika mapenzi.
JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU: Hakuna
jambo ambalo hutuliza fikra na hisia za mapenzi kama kukubali kumsamehe
yule aliyekuudhi kabla hata hajakuomba msamaha na kuamua kusahau yote
yaliyotokea. Yawezekana wengi mtasema haiwezekani.
Marafiki, lazima kila mmoja aelewe kwamba unapokasirika au
kuumizwa, anayeteseka siyo yule aliyekusababishia maumivu bali ni wewe
mwenyewe.
Hasira au maumivu ya kimapenzi huwa
kama moto mkali ambao huitafuna taratibu nafsi ya mhusika. Ukisamehe
maana yake unaupa moyo na akili yako nafasi ya kupata sehemu ya kutulia
na kuuzima moto ambao tayari ulishaanza kukolea ndani yako.
BADILISHA MAZINGIRA/ MARAFIKI:
Baada ya kuumizwa na mwandani wako, mbinu ya kubadilisha mazingira na
marafiki husaidia sana kukupa nguvu ya kukabiliana na msongo unaoweza
kukusababishia madhara makubwa.
Unaweza kubadilisha mazingira kwa
kusafiri, kubadilisha mpangilio wa chumba chako cha kulala na kuondoa
vitu vyote vinavyoweza kukukumbusha hisia chungu za maumivu. Taratibu
utaona akili yako ikianza kusahau maumivu.
Yawezekana pia kuwa mpenzi wako
ulishamtambulisha kwa marafiki zako nao wakamuona kama sehemu ya
familia. Ukiendelea kujumuika na marafiki hao, watakuwa wanakukumbusha
hisia chungu zitakazoendelea kukutesa, jiweke karibu na marafiki wapya
wasiojua historia yako ya mapenzi, watakuwa sehemu ya faraja kwako.
JIPENDE, JITHAMINI: Utafiti
wa kisaikolojia umebaini kuwa baada ya kutendwa kimapenzi, watu wengi
hujishusha thamani na kudhani huenda wana upungufu, kasoro au udhaifu
fulani ndiyo maana wapenzi wao wakawasaliti na kutoka kimapenzi na watu
wengine. Kama ni mwanamke, muda wote atashinda kwenye kioo akijikagua
kama ana kasoro kwenye sura na mwonekano wake. Mwanaume vivyo hivyo,
atashinda akijiuliza kuhusu uwezo wake wa kumfurahisha mwenza wake
faragha au uwezo wake wa kifedha.
Kujipenda na kujithamini kuende
sambamba na kuboresha mwonekano wako, hakikisha muda wote unakuwa msafi
na mazingira unayoishi pia yanakuwa masafi.
SITISHA MAWASILIANO:
Unapokuwa na maumivu ndani ya moyo wako, jambo la busara ni kukaa mbali
na kusitisha mawasiliano ya aina yoyote na yule aliyekusababishia
maumivu hayo. Wengi hufikia hatua ya kubadili namba zao za simu ili
kupata muda wa kutafakari mustakabali wa uhusiano wao.
Kama alikuwa rafiki yako kwenye
Facebook au Twitter, ‘block’ mawasiliano naye, kama ni kwenye simu
sitisha kumtumia ujumbe mfupi au kumpigiapigia simu, iache akili yako
ndiyo iamue kama bado unahitaji kuendelea kuwa naye au la.
USITAFUTE WA KUZIBA PENGO:
Kosa ambalo wengi hulifanya baada ya kutendwa na wapenzi wao, ni
kukurupuka na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na watu wengine muda mfupi
baada ya kuumizwa. Badala ya kupunguza maumivu, utajikuta ukiongeza
‘stress’ kichwani kwani huyo unayedhani atafaa kuziba pengo, anaweza
kuwa na maovu kushinda hata huyo aliyekuumiza.
Jipe nafasi ya kukaa mwenyewe na
kufikiria maisha yako ya baadaye, amini kwamba maisha yanawezekana hata
ukiwa peke yako, kubaliana na kilichotokea na jiambie kuwa hutaki
kurudia makosa kwa kuanzisha uhusiano na mtu atakayeuchezea moyo wako.
JIPE ZAWADI:
Huenda wengi wakashangaa kwamba inawezekanaje kujipa zawadi mwenyewe?
Inawezekana, tembelea duka linalouza zawadi za kimapenzi kama maua, kadi
nzuri, midoli au chocolate na jichagulie unayoipenda zaidi. Jiambie
kuwa hakuna anayekupenda zaidi ya jinsi unavyojipenda mwenyewe,
jipongeze kwani maumivu hayatajirudia tena.
Comments
Post a Comment