Chato Yatangaza Kiama cha Mapato
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chato mkoani Geita, Batholomeo Manunga amewataka madiwani kuwafichua
watendaji wa vijiji wanaoshirikiana na mawakala kuhujumu mapato.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha
baraza la madiwani, Manunga amesema baadhi ya watendaji wa vijiji na
kata wanahujumu mapato kwa kula njama na wazabuni.
“Hatutaendelea kuvumilia hali hii, na ni
jukumu letu sote kukabiliana na wote wanaohujumu mapato ya halmashauri
kwa sababu bila kuongezeka hatutaweza kuwahudumia wananchi waliotuamini
na kutuchagua,” amesema Manunga.
Bila kutaja majina wala kata husika,
mwenyekiti huyo alisema tayari halmashauri imegundua mtandao wa
wanaohujumu mapato ambao wataanza kushughulikiwa baada ya uchunguzi
kukamilika.
Amesema watu hao wamekuwa wakiihujumu
halmashauri hiyo na kuifanya ishindwe kutekeleza majukumu iliyojipangia
kutokana na fedha nyingi kuishia mifukoni mwao.
Manunga aliwasihi madiwani kuacha
kuwaonea aibu wezi wa mali za umma ili kuisaidia halmashauri hiyo kupiga
hatua kubwa ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Bwina, Sospeter
Nyamang’ondi ameishauri halmashauri hiyo kuwachuja mawakala wasiotimiza
wajibu na wanaoshirikiana na watendaji kuhujumu mapato.
Amesema iwapo mapato yatasimamiwa vizuri, halmashauri hiyo inaweza kukusanya zaidi ya Sh2 milioni kutoka kwenye mialo.
Diwani huyo amesema mapato mengi
yamekuwa yakiishia mikononi mwa watu wachache kutokana na kutokuwapo kwa
mikakati mathubuti ya kuwadhibiti.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Athanas Ngambakubi ameahidi kuweka mikakati kuongeza mapato na kubaini vyanzo vipya.
Amewaomba madiwani kushirikiana na
watendaji wa halmashauri kubaini vyanzo vipya vya mapato, ukusanyaji na
udhibiti wa mapato na usimamizi wa mapato ili kuiwezesha kutekeleza
miradi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment