Mwalimu Adaiwa Kumtia na Kumtoa Mimba Mwanafunzi.....
Mwalimu mmoja wa Shule Sekondari Nyugwa wilayani hapa Mkoa wa Geita anadaiwa kutoroka katika kituo chake cha kazi kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wake wa kidato cha tatu.Inadaiwa baada ya mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) kubainika kuwa na ujauzito, mwalimu huyo aliamua kushirikiana na baadhi ya watumishi wa Kituo cha Afya cha Kharumwa kutoa. Inadaiwa Machi 3, ndiyo mimba hiyo ilitolewa kwa ushirikiano wa daktari na muuguzi waliokuwa zamu.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa shule hiyo, Henrick Jembe alidai Februari 18, mwanafunzi huyo aliomba ruhusa kwenda hospitali akidai anaumwa.
“Ingawa sikuwapo shuleni siku hiyo, lakini kumbukumbu zinaonyesha mwanafunzi huyu alipewa ruhusu baada ya kukamilisha utaratibu ikiwamo kuandikiwa daftari la kumuwezesha kupatiwa matibabu,” alidai mkuu huyo wa shule na kuongeza:
“Alisindikizwa na wanafunzi wenzake wawili, mmoja wa kiume na mwingine wa kike.”
Alidai waliporejea shuleni, mwanafunzi huyo alisema baada ya vipimo alikutwa na vimelea vya malaria, hivyo akaruhusiwa aende nyumbani kupumzika.
“Lakini baada ya siku mbili nilipokea wito kutoka polisi nikitakiwa kufika na mwalimu anayetuhumiwa ambaye siku hiyo alikuwa na kazi ya kushughulikia chakula cha wanafunzi, ikabidi niende mwenyewe na kukuta maelezo kuwa mwanafunzi wangu ana ujauzito na anayetuhumiwa ni huyo mwalimu,” alidai Jembe na kuongeza:
“Nadhani alipopata taarifa kuwa anatuhuma hizo aliamua kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo.”
Katibu Mkuu Idara ya Utumishi wa Walimu wilayani hapa, Aron Andrew alisema baada ya kumhoji mwanafunzi huyo alibaini kuwa alianza uhusiano wa mapenzi na mwalimu wake tangu mwaka jana.
“Alisema baada ya kutolewa mimba, mwalimu wake alimsafirisha hadi jijini Mwanza kwa mtu aliyemtambulisha kwake kuwa ni dada wa mtuhumiwa ili ajiuguze huku akiendelea kunywa dawa alizoandikiwa hospitali,”
alisemaHata hivyo, alisema hawawezi kuchukua hatua yoyote dhidi ya mwalimu huyo kwa sasa kwa sababu wanasubiri taarifa kutoka kwa mwajili wa mwalimu huyo ambaye ni mkurugenzi.
Alisema mwajiri huyo akitoa taarifa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi mwalimu huyo kwa kuwa amekiuka sheria na kanuni za utumishi wa umma.Kaimu Mkurugenziwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Venance Ngeleuya alisema ofisi yake pia haijapokea taarifa za tuhuma hizo na kusisitiza watafuatilia.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Lutale Josephat alisema ofisi yake itachukuwa hatua kama itathibitika kuwa baadhi ya watumishi wa kituo cha afya cha Kharumwa walishiriki kumtoa mimba mwanafunzi huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Ibrahimu Marwa alisema amewaagiza polisi wilayani hapa kumsaka na kumtia mbaroni mwalimu huyo ili afikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya tuhuma zinazomkabili
Comments
Post a Comment