Mtangazaji Gadner Afunguka 'Ndoa Yangu na Jide Ilivunjwa Kwa Simu'



Mtangazaji nyota wa redio nchini, Gardner G. Habash ambaye hivi karibuni aliachana rasmi na mkewe Lady Jaydee (Judith Wambura Mbibo) kwa talaka iliyotolewa mahakamani, amesema ndoa yake ilivunjika kwa kupigiwa simu ikitokea nchini Marekani.

Katika mahojiano maalum yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Gardner alisema hata hivyo, licha ya kutengana kwao, yeye hana chuki na mwanamke huyo aliyeishi naye takriban miaka kumi mfululizo.

Yafuatayo ni mahojiano kamili:

RISASI: Kuna uhusiano gani kati yako na Jide (Lady Jaydee) baada ya kutengana?

GARDNER: Hakuna tunapokutana wala hatuna mawasiliano, kwa hiyo hatuna uhusiano japo mimi sina tatizo lolote wala uadui na yeye, hata hivyo sitashangaa yeye kuonyesha uadui maana ilivyotokea hivyo miezi kadhaa iliyopita.

RISASI: Miezi kadhaa iliyopita kilitokea nini unachotafsiri kama uadui?

GARDNER: Niliona dalili ya chuki wakati fulani nilimshauri tutoe tamko la pamoja kuhusu kutengana kwetu, sababu watu walikuwa wanatuuliza maana hawakutuona pamoja, hakukubali na akataka niwe nasema tu siyo kweli ni uzushi, tuko pamoja japo hatukuwa pamoja hivyo kwa ujinga wangu nilikubali na ndiyo maana nilikuwa najibu watu kuwa sio kweli.

Sasa siku niliyoshtuka ni kwamba mimi nilikuwa nazifuata akaunti zake za mitandao kama mtu niliyekuwa nasimamia kazi zake na niliendelea hivyo miezi kadhaa baada ya kutengana, kwanza nikaambiwa ameenda redioni kutangaza kuwa ameniacha huku mimi ameniambia niseme tu kuwa siyo kweli, ikawa aibu kwangu.

Halafu baadaye nikaona katika mtandao wake kaongea vitu ambavyo aliweka kama anajibu maswali aliyoruhusu aulizwe, lakini kwangu mimi ilikua shambulio, ndipo nilipotafsiri kuna chuki lakini mimi sitamchukia wala siyo adui yake. Kwa sasa ninashukuru talaka imepatikana na najua huu sio mwisho wa kupenda.

RISASI: Hivi ni nini hasa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yenu?

GARDNER: Chanzo anaweza kukisema yeye aliyekataa kuendelea na ndoa, mimi sikuwa na tatizo na yeye, ijapokuwa kutofautiana kwa hapa na pale katika ndoa ni jambo la kawaida, lakini sijajua hadi leo kipi kipya kizito kilifanya yeye atake kutengana.

RISASI: Kwani ilikuwajekuwaje sasa?

GARDNER: Nakumbuka ilikuwa Julai 2014, nilipata booking ya show yake aende kuimba Marekani, ilikuwa ni safari ambayo ingedumu kwa siku saba, lakini mimi nikamshauri akae mwezi mzima yaani aongeze wiki tatu zaidi baada ya show ili iwe ni likizo yake. Basi ilipofika wiki ya tatu ya mwezi huo, ndiyo akanipigia kuniambia akirudi hataki tena kuendelea kuwa katika ndoa.

RISASI: Ulijisikiaje baada ya kupata ujumbe huo?

GARDNER: Kibinadamu mtu umekaa naye miaka mingi ghafla akiwa safarini anakutaarifu kuwa hataki muwe wote tena wakati kaondoka mko sawa, na jana yake mmeendelea kuweka mipango ya maendeleo, nilijisikia vibaya na nilijaribu kutafuta maongezi, alikataa na hakurudi tena nyumbani, ikabidi kukubali ingawa kishingo upande. Nashukuru Mungu nikaanza upya nikaona maisha mapya.

RISASI: Unaweza kusema wakati unakutana na Jide ulimkuta akiwa na nini na wakati mnaachana ulimuacha na nini?

GARDNER: Si uungwana mimi kutangaza nilimkuta na nini labda aseme yeye, lakini tulizalisha mali za kutosha, tulikuwa na vyanzo kadhaa vya fedha na kwa bahati nzuri wewe ulikuwa karibu nasi uliona na wengi waliokuwa jirani nasi wanajua. Mimi nimelelewa kushirikiana na kushea na kamwe siyo kunyang’anyana, ndiyo maana sitasema mambo ya mali, kama kipo ninachostahili nt’akipata tu.
Ijapokuwa yeye amekuwa akipotosha watu kuwa mimi sikuwa na kitu, sikuwa na mchango wa kipato wala wa taaluma katika muda tuliokaa pamoja yaani ni kama Mario ninayemtumia na nilisikitika zaidi pale mahakamani Sinza hakimu alipomuuliza, ninanukuu ‘Kuna mali zozote mlipata wakati mko pamoja katika ndoa,? Yeye akajibu hamna. Hata hivyo mimi sijawahi kuonesha hata nia ya kutaka tugombee mali, nilimpa yeye aamue kila kitu ili kuepuka kulumbana lakini baadaye nikalipuliwa, hahahaha, najua mengi yatasemwa nipakwe ubaya.
Baada ya mahojiano hayo mafupi, gazeti hili lilimtafuta Jaydee na kufanikiwa kumpata kupitia simu yake ya mkononi.

RISASI: Mambo sista?
JAYDEE: Poa, nambie
RISASI: Mashabiki wa kapo yenu wangependa kujua nini hasa kilitokea katika ndoa yenu.
JAYDEE: Hivi stori moja mnaandika mwaka mzima? Kuna kipya gani hapo ambacho hamjaandika? Halafu kulikuwa na mashabiki wa Jaydee, hakukuwa na mashabiki wa couple.
JAYDEE: Hebu kuwa positive, kuna vitu vingi vizuri vya kuandika kuhusu mimi.

Comments

Popular posts from this blog

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 2 Exam Answers 100% 2016

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 3 Exam Answers 100% 2016

IT Essentials (ITE v6.0) Chapter 1 Exam Answers 100% 2016